Magonjwa Katika sura ya saba ulijifunza kuhusu kinga ya mwili. Pia, ulijifunza kuwa viini vya magonjwa hudhoofisha kinga ya mwili. Katika sura hii, utajifunza kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza. Utajifunza pia kuenea kwa magonjwa, dalili zake, na namna ya kujikinga. Magonjwa mengi hutokana na vimelea mbalimbali vilivyopo katika mazingira yetu. Vimelea hivyo huishi katika hewa, udongo, maji yaliyotuama, na chakula kisicho salama. Pia, vimelea hivyo hupatikana kwenye maji ya kunywa yasiyo salama. Vimelea hivyo huingia mwilini kupitia njia mbalimbali kama vile kinywa, njia ya hewa, na ngozi. Vilevile, magonjwa mengine hutokana na kugusana au kuumwa na wadudu wanaobeba vimelea vya magonjwa. Mfano, mbu jike aina ya Anofelesi huuma watu na kuwaambukiza vimelea vya malaria. Aina za Magonjwa Kuna magonjwa ya kuambukiza na magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa ya kuambukiza Baadhi ya magonjwa ya kuambukiza ni yale yanayowapata watoto chini ya miaka mitano. Magonjwa hayo ni kama vile: • Surua • Pepopunda • Tetekuwanga • Malaria • Kipindupindu • Kichocho • Kuhara damu • Homa ya matumbo • Kifua kikuu Magonjwa yasiyoambukiza Magonjwa yasiyoambukiza ni yale yasiyoenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Magonjwa hayo ni kama: • Saratani • Kisukari • Pumu • Shinikizo la damu • Kiriba tumbo Magonjwa Yasiyoambukiza Magonjwa yasiyoambukiza huweza kumpata mtu na kuwa naye kwa muda mrefu bila dalili zozote. Hali hiyo humfanya mtu asitafute tiba mpaka mwili unapoanza kuuma. Hivyo, inashauriwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara. Uchunguzi husaidia kugundua mapema kuwepo kwa ugonjwa mwilini na tiba ya mapema inapunguza uwezekano wa madhara zaidi. Saratani Saratani ni ugonjwa unaotokea kwenye chembe hai za mwili. Chembe hizo huanza kujigawa na kutengeneza chembe hai mpya bila mpangilio maalumu. Chembe hizi huendelea kukua kwa kasi na kutengeneza uvimbe unaoitwa saratani, ambao huweza kutokea sehemu yoyote ya mwili. Sababu za Saratani Saratani husababishwa na vitu mbalimbali vinavyoharibu mpangilio wa chembe hai za mwili kama vile: • Kemikali kutoka kwenye vyakula • Hewa chafu • Vipodozi • Dawa tunazotumia • Uchafuzi wa mazingira Namna ya Kuzuia Saratani • Kuepuka ulaji usiofaa • Kutotumia dawa kiholela • Kuepuka unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara • Matibabu ya mapema hospitalini Kisukari Kisukari husababishwa na mwili kushindwa kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu kutokana na upungufu wa homoni ya insulini inayotolewa na kongosho. Dalili za Kisukari • Kukojoa mara kwa mara • Kupungua uzito kwa haraka • Kuwa na kiu isiyoisha • Uchovu wa mwili • Hasira na kutoona vizuri • Vidonda kutopona haraka • Kupata ganzi mikononi au miguuni Namna ya Kuzuia Kisukari • Kufanya mazoezi ya viungo • Kudhibiti uzito wa mwili • Kufuata ulaji sahihi Pumu Pumu ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa upumuaji. Ugonjwa huu hujitokeza iwapo mtu mwenye ugonjwa atavuta hewa yenye viambata vinavyochochea ugonjwa kama vile vumbi, harufu kali, au chavua za maua. Dalili za Pumu • Kukohoa • Kupiga chafya • Kubanwa na kifua • Kushindwa kupumua • Kutoa sauti kama filimbi wakati wa kupumua Namna ya Kuzuia Pumu • Kujiepusha na vichochezi vinavyosababisha mzio • Kupata dawa kutoka hospitalini • Kuepuka mazingira na vyakula vinavyochochea mzio Magonjwa Yanayoambukiza Baadhi ya magonjwa ya kuambukiza hujulikana kama magonjwa ya mlipuko. Vimelea vya magonjwa haya husambaa kwa kasi katika muda mfupi na katika eneo kubwa, husababisha watu wengi kuathirika kwa muda mfupi. Magonjwa hayo ni: • Kipindupindu • Malaria • Kifua kikuu • Kichocho • Surua • Tetekuwanga • Pepopunda Malaria Kuenea kwa Malaria Malaria inaenezwa na mbu jike aina ya Anofelesi, ambaye huambukiza ugonjwa kwa kuingiza vimelea mwilini anapomuuma mtu. Dalili za Malaria • Baridi kali na kutetemeka • Joto kali mwilini • Kuumwa kichwa • Kutapika • Kupoteza hamu ya kula • Viungo vya mwili kukosa nguvu Namna ya Kuzuia Malaria • Kuharibu mazalio ya mbu kama vichaka, nyasi, na maji yaliyotuama • Kumwaga mafuta ya taa kwenye vidimbwi • Kuteketeza vifaa vinavyoweza kuwa mazalia ya mbu • Kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa • Kupata tiba mapema hospitalini Kipindupindu Kipindupindu ni ugonjwa wa mlipuko unaosababishwa na bakteria na huambatana na kuhara na kutapika mfululizo. Kuenea kwa Kipindupindu • Kinaenezwa na nzi wanaobeba kinyesi chenye bakteria kutoka sehemu moja kwenda nyingine • Kinaenezwa kwa kuchafua maji kwa kinyesi chenye viini vya kipindupindu Dalili za Kipindupindu • Kuharisha na kutapika mfululizo • Upungufu wa maji mwilini Namna ya Kuzuia Kipindupindu • Kutumia maji safi na salama • Kuhakikisha usafi wa vyakula na mazingira • Kufanya usafi wa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka chooni